MAISHA YA WANA WA MUNGU/ Pastor Dominick

UTANGULIZI
Mpendwa katika Jina la Bwana Yesu amani iwe kwako katika siku zako zote za maisha yako. Napenda kukushirikisha jambo la muhimu katika maisha yako ambayo tunapata katika Neno la Mungu kuhusu “maisha ya wana wa Mungu” Tunapata ukweli kuhusu namna ambavyo wana wa Mungu wanapaswa kuishi kwa maisha ya ushindi ya kibiblia wakiwa hapa duniani kama wapitaji. Wana wa Mungu ni akina nani? Biblia inatueleza wazi kuwa wana wa Mungu ni wale waliompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Yohana 1;12,13, “bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu,wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali ya Mungu. Tunaona kila mtu ambaye anafungua moyo wake na kumpokea Bwana Yesu kwa imani katika jina lake anaokoka na anapata uwezo wa kufanyika kuwa mtoto wa Mungu tena si waliozaliwa kwa mapenzi ya mwili na damu hizi tulizorithi kwa wazazi wetu ni kwa njia ya imani katika jina lake, neno la Mungu linasema katika Galatia 3:26,27“kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika kristo yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika kristo mmemvaa kristo.”Tena katika 1petro 1:23,24 kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikaya,bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima lidumulo hata milele……Mpendwa katika jina la Yesu hawezi mtu kuwa mwana Mungu isipokuwa amezaliwa mara ya pili kwa neno la imani katika jina la Yesu. Kwa nini kuishi katika maisha yasiyofaa? Hali wewe ni mwana Mungu. Umehubiriwa neno la imani ambalo laweza kubadilisha maisha yako na kuwa mtoto mtiifu wa Mungu, Warumi10:8 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako;yaani ni lile neno la imani tulihubirilo.Namshukuru Mungu kwa neno hilo kwa sababu linatuambia ukiamini moyoni na kumkiri Yesu kuwa ni Bwana unahesabiwa haki na kupata wokovu kwa sababu hiyo unapata sifa ya kuitwa mtoto wa Mungu, maana Yesu amekufa akafufuka kutoka kwa wafu amepaa mbinguni na ameketi katika kiti cha enzi na anatuombea kwa baba ili tushinde dunia hii na maovu yote yaliyomo humu. Kwahiyo neno lake linapoanguka moyoni mwako linakubadilisha na kukufanya mtoto wa Mungu na kusafishwa kwa damu ya Yesu kwa kusamehewa dhambi.

Mpendwa msomaji katika jina la Yesu baada ya kujifunza kuwa mtu anafanyikaje kuwa mtoto wa Mungu basi sasa tujifunze mambo ya muhimu kujua na kuzingatia kuyashika na kuishi nayo katika maisha yako. Naamini Mungu atakusaidia kuona siri fulani amabayo itainua imani yako juu ya Mungu na mafanikio ya maisha katika viwango mbalimbali katika imani. Nakuahidi kuwa hutakuwa kama awali kabla hujasoma kitabu hiki naomba Mungu akupe macho ya rohoni uone siri hii. Katika sehemu kuna mfululizo wa mambo yafuatayo;

• kuishi kwa imani

• kuwa na upendo wa Mungu

• kuwa mtii na mwaminifu

• kufanya maombi na maombezi

• tumepewa mamlaka na Mungu

Twende kwa pamoja tujifunze vipengele hivyo kwa umakini upokee muujiza wako katika jina la Yesu kristo Mungu akutie nguvu amina:

Kuishi kwa imani

Mpendwa mtoto wa Mungu kwa njia ya Imani katika jina la Yesu tunapaswa kuishi kwa imani kwa sababu ukimpokea Yesu una uzima wa milele 1yoh 5:13 neno linasema “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue kuwa mna uzima wa milee,ninyi mnaoamini jina la mwana wa Mungu. Kama tulivyotangulia kuona kuwa hakuna anyeweza kuwa mwana Mungu bila ya kuamini ( Yesu) jina la mwana pekee wa Mungu. Yoh 3:18 anasema “ amwaminiye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha hukumiwa; kwa sababu hakuamini jina la mwana pekee wa Mungu.kwa sababu hiyo kuamini jina la Yesu ni lazima katika maisha ya wana Mungu kwani asiyeamini hujikuta hukumuni.hivyo tuamini jina hili ili tuishi maisha ya ushindi hapa duniani na kuingia ulimwengu ujao.kuna kitu cha zaidi unapoamua kuishi maisha ya imani ilyohai amboyo ina sifa ya kukua na kuongezeka. Imani ni nini? Imani ni kuwa na hakika ya mambo ya tarajiwayo,ni bayana ya mambo yasiyonekana. Ebrania11.1 kama neno la Mungu linavyosema kama mtu hana uhakika wa mambo yasiyonekana sasa hana imani. Hebu tufikiri kidogo Mungu angeanza kuumba ulimwengu kwa vitu vinavyoshikika na kuonekana angepata wapivitu kama mawe, miti maji , angepata wapi hivyo vitu? Maana havikuwepo. Kwa hiyo Mungu aliamini kwanza ndipo akatamka vitu vyote vionekanavyo na visivyonekana; ulimwengu na vitu vyote vikaumbika na kuoneka pia vinashikika. Soma vizuri Ebrania 11:1-38 mpendwa msomaji Mungu aliyeahidi ni mwaminifu sana atafanya. Kama unataka kupata imani juu jambo fulani unalolitaka lazima ujue Chanzo cha kupata imani ambayo nikusikia neno la Munguwarumi 10:17 basi imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la kristo. Kwa hiyo kama nikitaka imani juu ya jambo fulani kwa Mungu lazima nipate mbegu ambayo ni neno la kristo na niandae shamba (moyo) kwa sababu neno la kristo nimbengu ya kupatia imani na mioyo yetu ni shamba luka 8:11 “Na huo mfano,maana yake ni hii mbengu ni neno la Mungu. Yesu amesema neno ni mbegu ikipata shamba lenye rutuba yaani moyo uliomwelekea kwa kumaanisha huota na kukua. Paulo mtume alieleza hili kwa wakorintho1kor3:9 Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi shamba la mungu,ni jengo la Mungu. Paulo anasena mimi nilipanda Apolo alitia maji akuzaye ni Mungu. 1kor 3:7. Mpendwa mtoto wa Mungu andaa moyo wako kwa kupokea ahadi za Mungu na kuichanganya na imani utaona matokeo mazuri katika maisha yako ya wokovu, hakuna haja ya kuwa na mashaka juu ya yale aliyoahidi, maana yeye ni mwaminifu na wa haki.

hesabu 23:19,20

Mungu si mtu, hata aseme uwongo;

Wala si mwanadamu, ajute;

Iwapo amesema, hata hatatenda?

Iwapo amenena,hatalifikiliza?

Tazama, nimepewa amri kubariki,

Yeye amebariki,nami siwezi kulitangua.

Mpendwa katika jina la Yesu iwapo Mungu amesema,ameahidi, hatatende? Ameahidi uponyaji,baraka,miujiza, kukuinua , makao ya milele, na ahadi nyingi sana katika neno lake lakini hatuoni matokeo kwa kutokuziamini ahadi za Bwana na kutokuwa tayari kuzipokea. Imani chanzo chake ni kusikia hata sasa umesoma neno inua imani yako utoke katika hali uliyonayo simamia ahadi za Mungu kama mashahidi wengi wanaotajwa katika biblia ebrania 11 kwakuziamini ahadi za Mungu walishuhudiwa kuwa Mungu yupo na anawapa thawabu wale wamtafutao. Mpendwa msomaji kuna ahadi nyingi naziona juu yako, nakutia moyo kuwa saa imefika kuachana na imani haba, iliyokufa, na kushikamana na imani hai na inayokua ambayo ina matendo yakobo 2:18

Hebu tuangalie mfano mashujaa wachache katika biblia walioamua kuishi kwa imani,na kupokea kile walichotarajia kwa Mungu

HENOKO ALIISHI KWA IMANI

Henoko ninayemtaja ni mwana wa Yeredi, mwana wa Mahaleli mwana Kenani mwana, wa Enoshi mwana Sethi mwana Adamu mwana Mungu. Mwanzo 5;1-22Henoko alishi miaka mia tatu na sitini na tano. Kwa imani kama neno linavyosema mwenye haki wangu kwa imani ataishi. Ebrania 10:38 “lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani”Hata kama mateso,adha,shida,magonjwa, umaskini,dhambi,kukatishwa tamaa,huoni njia ya kutokea tunaishi katika nyakati ngumu kama ya nabii Habakuki tunashinda na kupokea ahadi zetu kwa imani. Habakuku 2:2-4 usisahau Henoko aliishi katika dunia ilijaa maovu katika ujana wake hata alipotwaliwa na Mungu; kwa muda wote miaka mia tatu na sitini na tano aliishi kwa imani tunasoma Ebrania 11;5 “ kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti ,wala hakuonekana, kwa sababuMungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.”Kumbuka Henoko aliishi katika dunia ambayo Mungu alishatamka laana kwamba mwanadamu baada ya kuishi lazima arudi ardhini; lakini Imani ya Henoko imemfanya anyakuliwa na Mungu amen. Mpendwa imani inayoishi itakuto nje ya mazingira magumu. Hata mimi na wewe tuishi kwa imani na utakatifu tutaishinda dunia hii ambayo imejaa maovu na dhuluma

IBRAHIMU ALIISHI KWA IMANI

Ibrahimu alipoitwa na Mungu, ana umri wa miaka sitini na mitano kutoka katika Uru ya Ukaldayo, na kwenda katika nchi ya Kanaani asiyoijuayeye ila Mungu pekee aliijua. Kwa kuwa alimwamini Mungu aliitikia akaondoka; yeye na mke wake Sarai na Lutu mwana wa ndugu yake. Si jambo rahisi kuondoka na kuacha jamaa yako na kwenda katika nchi ya ya ugenini ambayo huna mwenyeji lakini kwakuwa alimwamini Mungu aliondoka kwa imani ebrania 11:8 “ kwa imani Ibrahimu alipoitwa alitoka aende mahali pale atakapopata kuwa urithi alitoka asijue aendako.Kuna mahali hata wewe hupajui lakini Mungu anataka utoke ulipo na uende mahali pa urithi wako yaani ngazi nyingine ya mafanikio na ustawi wako kiroho, kimwili, kiuchumi, ndoa yako,masomo yako, afya yako na hata maeneo yote ya maisha yako. Mimi na wewe Bwana anatuita tutoke katika ngazi tuliyonayo je! Uko tayari? Kama uko tayari shangilia ahadi za Mungu kwa kusema “ HALELUYA” kumbuka Ibrahimu alikaa muda mrefu kupokea ahadi za Mungu lakini hakukata tamaa kwa sababu alimwamini Mungu. Kwa mfano suala la kupata mtoto limekaa muda mrefu bila kukamilika hata tumbo lake Sarai mkewe Ibrahimu likafa kwa mabo ya kupata mimba. Lakini kwakuwa walimwamini Mungu walishangilia ahadi za Mungu na kuziamini ebrania 11:9-19. Nawe mpendwa mwana wa Mungu kwa njia imani katika jina laYESU; sauti ya baba yako inakuita kwa upole uingie katika mfumo wa maisha ya baraka ambayo Mungu ameawaandalia watoto wake. Waefeso 2:10. Maana tu kazi yake, alituumba katika kristo Yesu, tutende matendo mema, abayo tokea awali Mungu aliumba twende nayo.Hvyo inawezekana unaishi chini ya kiwango ambayo Mungu amekupagia ni imani tu amboyo inaweza kutoa hapo ulipo usonge mbele na safari ya mafanikio.

Hebu tuone baadhi ya ahadi za Mungu ambazo ameahidi kwa Ibrahimu na uzao wake. Uzao wa Ibrahimu nao ni namna mbili kuna wale wa waliozaliwa kimwili yaani Wayahudi na wazao wa Ibrahimu kwa Imani. Galatia 3:7 “fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Kataka mstari wa 3;9 anasema “Basi walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahamu aliyekuwa mwenye imani.

 Mungu alimwahidi Ibrahimu mtoto ambaye atakuwa baraka kwa matifa yote, Mungu akatimiza ahadi yake. mwanzo 15:4-6

Kumbuka tunajifunza wana wa Mungu kuishi kwa imani, Ibrahimu katika maisha yake baada ya safari ndefu ya kusubiri ahadi ya Bwana katika nchi asiyoijua awali, ahadi ya Mungu ikatimia kwake. Nawe mpendwa amini ahadi za Bwana utapokea.

 Ibrahimu alipewa ahadi ya kuridhi nchi, kumbuka tunaposema nchi inamaana ni eneo lenye mipaka yake. Mungu akamwita Ibrahimu toka katika nyumba ya baba yake na kwenda katika nchi ambayo inakaliwa na wengine lakini kwa kuwa alimwamini Mungu aliitika na kutii sauti ya Mungu hivyo akapata nchi ya Kanaani kuwa uridhi wake. Nawe mpendwa unayeishi kwenye ardhi, nyumba, shamba, gari na kazi isiyokupa pato nyenye mafanikio mwamini Mungu, utazipokea ahadi kutoka kwa Mungu.

 Atakuwa taifa kubwa, mwanzo 12:2 “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa na kukubariki,kulikuza jina lako; nawe uwe baraka. Mungu alimwahidi hayo yote tuliyoona hapo juu imekuwa kweli ikatimia leo kwa wayahudi wamekuwa baraka kwa kila taifa duniani.

Mpendwa kwa mfano wa Henoko na Ibrahimu naamini umeinuliwa imani yako na kuziamini ahadi za Bwana na kusubiri pale unapohisi kuwa imechelewa. Lakini Mungu achelewi kutimiza ahadi yake kwako, huta kufa utaishi kwa imani mpaka kusudi la Mungu itakapotimia hapa duniani na uzima wa milele ujao

KUWA NA UPENDO WA MUNGU

Upendo ni hali ya kitu kupewa nafasi ya heshima ndani ya moyo wa mtu/hali ya kuthamini kitu inakuwepo ndani ya moyo wa mtu apendaye. Ni uhusiano wa kujitoa nafsi kwa ajili ya mwingine. (Yoh. 15:11-13).

Kumuona mwingine bora kama wewe mwenyewe au kumuweka katika nafasi ya kwanza baada yako kuliko kitu kingine. (1Yoh. 3:1)

Kumuweka mwingine kwenye nafasi yako kiuthamani. (Mt. 7:12)

Kuutoa uhai kwa ajili ya mwingine kwa sababu ya kumthamini sana (1Yoh. 3:16).

Kutenda jambo kwa ajili ya mwingine bila kutarajia/kungojea – malipo/mshahara.

Kutenda mema kwa wengine hata kama unaumia au hata kufa, kwa sababu unamuona yeye ni wa thamani sana.

Ni kuvutiwa na kumuona mwenzio anapendeza sana mbele ya Mungu na mbele yako kwa jinsi alivyo! (1Sam.19:2)Kuna aina nyingi za upendo hivyo lazima tubaini hasa ni upendo gani huu tunaosisitizwa wana wa Mungu tuwe nao katika maisha yetu. (EFE 3:14-15) 1) Upendo Wa Ki / Mungu –Agape (Agapen = Kupenda)

a) Mungu kwa mwanadamu/Viumbe.

i) (Yoh. 3:16)

ii) 1Yoh. 3:1

b) Mwanadamu kwa Mungu.

c) Mwanadamu kwa mwanadamu.

i) Kirafiki

ii) Kikanisa

iii) Kindugu/kifamilia.

(1) Mume na mke

(2) Mzazi na mtoto

(3) Kaka na dada / Kaka na kaka.

(4) Upendo kwa Adui

(1Sam. 18: 1Sam. 19: 2)

SIFA NA TABIA ZA UPENDO WA KIMUNGU. (1KOR.13:1-13.)

1) Ni upendo wa milele. (Yer.31:3 )

2) Una nguvu sana kuliko mauti (Wimb.8:6)

3) Ni wa thamani kubwa sana isiyopungua, hauzimiki (Wimb.8:7)

4) Ni karama iliyo kuu kuliko zote, katika karama za masaidiano (ya kurehemu na kukirimu) – lakini karama zote ni bora hakuna iliyo bora zaidi ya nyingine.(Yoh.13:34)

5) Ni amri kuu kuliko zote

Ni amri mpya ambayo kanisa limepewa na BWANA Yesu Kristo

6) Haubagui

Hauna mipaka, hauzuiliki, haubagui

Hauna, ukabila utajiri, wala cheo.

7) Unavumilia yote (una saburi). 1Yoh.4:18)

Haukati tamaa,

Hauna papara-harakaharaka,

Haulipizi kisasi,

Una upole-si mwepesi wa kuadhibu au kulipiza kisasi,

Hauna hila, mambo ya kukomoana

Una utaratibu-mpangilio wa mambo;

Unafadhili –Husaidia wahitaji .

9) Hauna husuda

hauyakasirikii au hauyaonei wivu mafanikio ya mwingine, hauonei chuki au hasira mafanikio ya mwingine. (Hes. 11:25-29, Yoh. 3:22-29, Mk. 9:38-40).

10) Hautakabari (Takabari=Kiburi; Takabali=Kubali).

Hauna kiburi au kujiinua na kujisifu.

Hauna ‘lakini mimi bwana…’ au …bila mimi na… yule si kitu’.

Unamhesabu kila mtu kuwa ni kiungo muhimu sana katika kanisa.

Huyachukua mabaya yote kuwa ni mimi ndiye sababisho na si mwingine.

Hivyo hauwalaumu wengine.

11) Haujivuni.

Haujioni au kujihesabu kuwa ni bora kuliko wengine. Haujitangulizi kuliko wengine-Luk.18:9-14.

Huona mafanikio yote ni Mungu aliyeyafanya na wengine, hatakama yeye ni muhusika mwenyewe. (Luk. 17:10.)

Hauwachongei – hauwashitaki wakosaji mbele za Mungu.

12) Haukosi kuwa na Adabu.

Unamuweka kila mtu katika nafasi anayostahili.

Unampa kila mtu haki yake. (Rum.13: 7)

Maneno ya Adabu,

Matendo ya adabu

Una nidhamu -hufuata utaratibu.

13) Hautafuti mambo yake

Hauna Ubinafsi.

Haujitafutii faida yake tu, bali unawafikiria wengine.

Unawatanguliza wengine.

Unajitoa nafsi yake kwa ajili ya wengine.

14) Hauoni Uchungu.

Hauna Kinyongo, kisirani, hauziri.

15) Hauhesabu mabaya (Zab.32:1-2, Mt.18:21-35).

Hauangalii upande wa mabaya tu.

BWANA kama Wewe ungehesabu makosa ni nani angesimama? (Zab.103:3).

16) Haufurahii udhalimu.

Haufurahii makosa / ukosaji / uongo / upotovu.

Haufurahii mwingine ateseke au apatikanapo na mabaya.

Uko tayari kubeba mateso hayo ili mwingine apone naam, hata maadui wake!

17) Hufurahi pamoja na kweli.

Baada ya kuona aina za upendo, mpendwa mwana Mungu uliyeokolewa na kusamehewa dhambi kwa upendo mkuu alionao Bwana wetu Yesu kristo kwetu Yohana 15:9-13 Kama vile baba alivyonipenda mimi, name nilivyowapenda ninyi,kaeni katika pendo langu. ……Amri yangu ndiyo hii, mpendane, kama nilivyo wapenda ninyi…… kwa hiyo mpendwa upendo huu wa Agape yaani upendo wa kimungu ndiyo unaotufanya tuwapende wale wanaotutesa, maadui zetu, wanotuteta na kututakia mabaya, kama wewe ungekuwa Stephano ambaye anauawa kwasababu amewaletea habari njema kwao unefanyeje kwa waompiga? Mdo 7:54-60 …….Akapiga magoti,akalia kwa sauti kuu, Bwana usiwahesabie dhambi hii…..Mpendwa unaonaje kama wewe utakuwa shujaa kama Stephano shemasi wa kanisa la mwanzo alivyofanya, nawe wasamehe wale wanaokuudhi ili nawe upokee ushindi kama Yesu alivyo tuagiza kusamehe wale wanaotukosea? Basi twende tuone mtu mwenye upendo wa Mungu ana sifa gani?

 Mwepesi wa kusamehe na kusahau kwa Yule aliyekusea, hivyo unasamehe kwa faida yako, siyo kwa faida ya yaule mkosaji wako. Kama ukisamehe nafisi yako inakuwa huru kuwaza mambo mengine ya faida kulikokuwaza mtu. Lakini pia sifa ya wana Mungu ni msahaha kama baba yao alivyo mwingi wa rehema na msamaha. Mpenwa mwachie aliyekosea asiwe moyoni mwako kwa chuki bali kwa upendo ili uwe mtakatufu kama baba yako alivyo matakatifu. 1pet 1:16-25. (Naomba chukua biblia soma mistari hiyo)

 Mwombaji, kuwaombea wale wanaokuudhi na kuomba toba kwa ajili watu wote; lakini maobi ya mtu wa namna hiyo husikilizwa na kujibiwa haraka sana kuliko maombi ya mtu kama Kaini mwana wa Adamu, mwanzo 4:7-9 Mungu alimwambia Kaini kuwa kutenda vyema hutapata kibali? Lakini kwa ukaidi aliamua kumwua ndungu yake asiyekosa kumbe kilichokuwa kinamsumbua siyo ndungu yake bali ni dhambi ilikuwa moyoni mwake. Mk 11:24-26. Kama wewe utamsamehe ndungu yako na mungu hatasikiliza makosa yako, hivyo masamehe ndungu yako kwa kuwa unampenda. Ili kusistiza hili naomba tusome 1kor13 baada ya kusoma utaona kuwa Paulo kwa uwezo wa Roho mtakatifu anatuagiza upendo ndiyo kipimo cha mwana Mungu asipokuwa na upendo atakuwa si kitu kabisa. Hivyo ni matumaini yangu kuwa sasa uko tayari kuishi katika upendo wa Mungu, ili Bwana atakaporudi atukute salama kwani tusipoishi kwa upendo hatuna sifa ya kuitwa wana wa Mungu. 2kor 6:14-18 Msifungiwe nira na…………………

KUWA MTII NA MWAMINIFU
Utii, ni hali ya kutekeleza maagizo uliyopewa na mtu mwenye mamlaka bila kupindisha, hivyo kila mtoto wa Mungu anapaswa kuwa mtiifu. Uaminifu, ni hali ya kutunza na kutekeleza makubaliano au maagano kati ya pande mbili. Kwa hiyo utii na uaminifu ni sifa mbili zinazotegemeana ambayo mtu au jamii ya watu wanapaswa kuzingatia katika maisha ya kila siku. Kumb 28:1-15 Mungu aliwaambia waisrael kuwa watii na kuwa waaminifu kwa maagizo yake yote. Yakobo 4:7,8 anasema Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ,enyi wenye nia mbili. Mpendwa mtoto wa Mungu wewe ni wa maana sana mbele za Mungu hivyo uishi katika hali ya utii na uaminifu ili Mungu awe katika maisha yako ili utakapotimiza maagizo hayo, Mungu aachilie baraka katika maisha yako ya sasa na ya baadaye.watu wengi wamekosa baraka za Mungu kwa sababu ya kutokuwa waaminifu na watii katika neno la Mungu na wanafuata njia zao wenyewe na kuacha njia za Mungu wao, hivyo wamejikuta katika mitego mingi ya shaeteni.hvyo nyenyekea chini ya mkono wa Mungu ili atukweze kwa wakati wake, kwani Mungu akiwa upande wetu hakuna aliye juu yetu.Rum 8:31-39.Zab119:9.ewe kijana uko mwujiza wako mbele tii uone mkono wa Mungu katika maisha yako.maombi yangu kwa Mungu aliye hai akukuse moyo wako ili tuishi maisha ya utii na uaminifu; katika ndoa, ujana wako, kazi ya Mungu uliyopewa,katika utoaji wasadaka,mafungu ya kumi, kazi ya serikali na hatakwa mali ya wengine. Naomba tuone mifano ya watumishi wa Mungu ambao walikuwa ni waaminifu;

YUSUFU MWANA WA YAKOBO

Yusufu tunayemzunguzia ni mwana wa Yakobo alikuwa mzaliwa wa kwanza kwa Raheli na Yakobo, alikuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mungu kwa wazazi wake alipokuwa mdogo alikuwa mwana mtiifu kwa babaye, na alikuwa anaeleza maovu ya ndugu zake kwa baba yake. Mwanzo 39:1-13 alikuwa mwaminifu wakati mke wa Potifa alipomshawishi kuzini alikataa.alikubali kwenda jela bila kuvunja uaminifu wake.lakini baada ya jaribu lile aliinuliwa kuwa mkuu katika nchi ya Misri na kuwa msaada kwa taifa lile.mpendwa mwana wa Mungu uwe mwaminifu katika maisha yako ili uinuliwe wewe katika maisha yako.

KUFANYA MAOMBI NA MAOMBEZI

Mpendwa mwana wa Mungu maombi ni mazungumzo kati ya mwana na baba yaani Mungu, ili awape mahitaji ambayo mtoto wake anahitaji. Hivyo Mungu anategemea watoto wake waliooko duniani waombe ili atende mambo makuu.Bwana yesu alisema imewapasa kumwomba Mungu siku zote bila kukata tamaa. Mathayo7:7 ombeni,nanyi mtapewa;tafuteni,nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa. Mpendwa mwana wa Mungu vitu vingu hatupati kwa sababu nyingi zikiwemo zifutazo;

 Kutokuomba, hii ni sababu inayotokana na mtu kutokujua nafasi aliyonayo ambayo amepewa na Mungu kuwa ni mtoto wake.hivyo unajidharau kuwa Mungu hawezi kukusikiliza mtu kama wewe basi unaacha kuomba kabisa; hili hii ni ya hatari sana kwa maisha ya kiroho, kwani unamekata mawasiliano na makao makuu. Yakobo 4:2 hivyo inatupasa kuomba kwa bidii ili Baba atupatie tunayohitaji.

 Uhaba wa imani katika maombi, Ebrania 11:6 lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini yeye yuko na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. Kuamini ndani ya moyo kuwa Mungu yuko na anaishi milele aliyetenda zamani ndiye anayetenda hata sasa katika maisha yetu. Mwite leo katika hitaji lako, shida, njaa, karo za shule, magonjwa, vita,na mambo mengine mengi sana; yeye atakupatia yote unayohitaji.

 Kutokuwa na utii kwa Mungu;watoto wasio watii kwa wazazi wao si rahisi kupewa vitu wanavyohitaji; Isaya 1:19. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; mpendwa mimi na wewe kama tukikubali na kutii kama neno la Mungu hakika tutakula mema katika dunia hii na uzima wa milele pia, kwa mfano neno la sema katika Isaya57:14,15.anaseme kuwa “naye atasema,

Tutieni, tutieni,

Itengenezeni njia,

Kiondoeni kila kikwazacho

Katika njia ya watu wangu.

Maana yeye aliye juu ,aliyetukuka, akaa milele;ambaye jina lake ni mtakatifu; asemsa hivi nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea,ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kufufua mioyo ya yao iliyotubu. Mpendwa mtoto wa Mungu,utii una sehemu kubwa sana katika kujibiwa maombi yako; utii wa neno la Mungu na roho iliyotubu na kunyenyekea hapo Mungu anaachilia baraka zake katika maisha yako na kujibu maombi yako ili upokee kile unachohitaji. Basi mtii Mungu kwa mali, mfano mafungu ya kumi, malimbuko yaani mazao ya kwanza ya mashamba yako na mifugo wako. Kwa mwili wako pia kwani wewe si mali yako mwenyewa bali nai mali ya Mungu.